Search This Blog

Saturday, February 5, 2011

GOMBA LA TAXI

Jana nakaa markiti namngoja mtu, nikipeleka macho naona jamaa watatu waja kila mmoja amefurisha tavu kwa taqsimu. Macho yamewakoboka wako wangu wangu kwa nakhwa. walipofika kuna taxi wakaingiya. Moja akaa mbele wawili wakakaa nyuma.

Dereva wa taxi akawaangaliya akajuwa leo mmeru yuko mjini.

"Jamaa mwaendapi?" Dereva akawauliza.

"Wewe twende tu!" Wakamjibu.

Dereva akawasha gari, akalingurumisha, kisha akalizima.

"Haya, tushafika!" Akawaambiya.

Wale wa nyuma kila mmoja akanyosha mkono wakampa pesa hao wakashuka.

Yule wa mbele akamgeukiya, akampiga kibao kimoja murwa kabisa kisha akamwambiya "We mpumbavu sana wewe!" alafu akashuka.

Nikajiambiya si haba angaa gomba halijamshika.

Akageuka akanambiya "Shoga sana yule, apeleka gari mbio ataka tuuwa!!!" huku yuwenda zake.

Friday, February 4, 2011

PILAU MOTO MOTO

Raha ya Ijumaa ni baada ya swalaa waenda piga pilau yako kwa kachumbari, pili pili ya kukaanga na jagi la juice. Hatupendi matanga lakini pia napo kuna pilau tamu!

Siku hiyo tulikwenda kuzika, baada ya mazishi tukarudi kulikofiliwa kupiga pilau yetu. Siniya zikaletwa moto moto. Ikawa siniya moja watu watatu. Nimekaa mimi, Mwamadi na Abduli

Pilau haidariki sura ilivyomoto lakini nikimwangaliya Abduli abugiya utasema ana friji mdomoni. Apiga matonge hakuna imani.



Mara twamuona Abduli amenyamaza kimya hali tena amwaga machozi tu. Wacha tuanze wasi wasi.

"Abduli una nini?" Jamaa wamuuliza.

Hajibu kitu azidi kuliya. Watu wakaanza wasi wasi kweli.

Baada ya kama dakika tano akafunguwa mdomo atwambiya kwa maskitiko "Poleni jamaa, kifo cha leo kimenikumbusha marhemu nyanyangu!"

Ikabidi tumsubirishe tumwambie ndio mambo ya kiduniya. Akanyamza akendeleya kula.

Tukitoka nje twaenda zetu mara anambiya "Wajua nini? Hakuna cha marhemu bibi wala ukwaju! Nilikuwa nimemenya kiazi moto kama kaa! Kimeniambata kwenye meno na mafinzi! Kukimiza siwezi na kukitema siwezi!"

Thursday, February 3, 2011

MKEBE

Charo alinisumbuwa kweli ataka kazi, nikampeleka kwa jamaa yangu akapewa kazi ya kuangaliya garden.

Akaingiya makazi akapewa mzee aitwa Bakari akaambiwa ukitaka chochote wewe muone Bakari atakusaidia.

Baada ya muda Charo tumbo likamuanziya balaa, akaenda kwa Bakari kumuuliza choo kilipo. Bakari akamuonesha choo akamwambiya mfereji uko khatuwa kadhaa na chooni, atachota maji ndio aende nayo chooni.

Charo akatafuta mkebe alipopata akaenda mferejini kuchota maji akarudi na kuingiya chooni. Alipomaliza ataka kutamba, akipiga jicho mkebe hauna maji! Loh! Akatafuta tafuta namna akajisafisha huyo akarudi kazi. Alipomuona Bakari akamweleza,


"Yaonesha huo mkebe una shimo dogo maji yavuja pole pole." Bakari akamwambiya.



Siku ya pili Charo yuko kazini akashikwa tena na haja akaenda akatwaa ule mkebe wake akaenda chota maji akarudi nao choni. Mara huyo yuwaja mbio kwa Bakari acheka kweli,

Amwambiya, "Bwana Bakari, rero mkebe nkauweza! nkatamba, nkatamba kisha ndipo nkanya!"

Wednesday, February 2, 2011

Ya matatu ni mengi

Matatu zina vituko shekhe; Zenye midundo utasema waskizishwa waliyoko njiani hata si wale walio panda, kuna nyengine umekaa kwenye kiti lakini waona lami ukiangaliya chini. Si muhimu ni kufika bwana.

Juzi nikapanda matatu nikakaa upande wa kushoto, kule mwisho upande wa dirisha amekaa mwanamke chuma! amepakata mtoto, kisha kati kati yetu amekaa kijana apata kama miaka ishirini.

Matatu yenda mara kitoto kikaanza kuliya. Yule mwanamke akamlaza akamtoleya mtoto nyonyo pengine atanyamaza. Nilishtuka manake si kawaida sehemu hizi za kwetu mwanamke kutowa titi mahali popote, na hata akitowa atajifinika kwa nguo.

Mwanamke akesha kumbembeleza mtoto anyonye lakini wapi!

"Chukuwa nyonyo ama nitampa huyu mvlana ale yeye!" Ikabidi amtishie mali yake ili apate kunyonya.

Doh, nikashtuka maneno gani haya tena. Lakini ukimwangaliya mwana alivoleta zani utaelewa. Ikibidi imebidi sio?

"Nakwambiya baby nyonya ama nitampa huyu!!!" akarudiya mara ya pili.


Wapi! Nataka kumwambiya huyo mtoto pengine amechuchu, ama aumwa, hana haja kunyonya lakini nasema haina haja wacha nitazame yangu.

"Usiponyonya nitampa huyu nakwambiya!!!!" akamwambiya tena.

Wacha jamaa aje kali, "Sister kama utanipa nipe bwana sio kusema tu! Mi nishapita steji yangu kitambo nakungoja wewe uamuwe! Unkazana nitampa, nitampa! Wanipa ama hunipi nishuke?"

Ilibidi dereva aongeze mdundo, si mambo haya!

Tuesday, February 1, 2011

IMETOKA AMU


Mbona mtu akienda majuu - London, USA, Canada – akirudi huku huwa lugha imebadilika? Jamaa akizungumza maneno mawili basi la tatu ni “Yes”, “No”, ama atatiya neno la kizungu ili mradi tu.

Sasa kuna na hawa yakhe wengine wakifika Nairobi na wao wataka kuzungumza Sheng (lugha ya mtaani ya Nairobi).  Basi Famau Alhamdulillahi akafika Nairobi akawa apiga kibaruwa. Baada ya muda akapoteya haonekani kumbe amerudi zake visiwani.

Siku hiyo niko Mombasa na Jemo rafiki yangu wa kinairobi muda namshtukiya Famau huyu ndiye!

“Ah Famau abawa, assalam aleikum! “ Namwakuwa kwa furaha

Sikujuwa kumbe Jemo na Famau wajuana.

“Ah Famaa, niaje budaa! Mzee ulilostiya Costo kumbe!” Jemoo akaruka kumuamkuwa.

“Niko mazeee, nirudi mahomuuu!” Alaa? Famau azungumza sheng?

“Manze kuna day nilikuvutiya wire lakini rununu iko mteja, kwani ulichange number?” Jemo akamuuliza.

“Simu yangu nilijepewa joooo!”

Ah! Famau! Jepewa???

NYUNYIZA JIJI

Siku hiyo nimefwatana na swahibu yangu maeneo ya viwanadani Nairobi; wenye jiji wakuita Indaa. Mbona siku ilikuwa inda. Jamaa amekabwa na mkojo anikazanisha mwendo ati atafuta choo utasema mgonjwa wa sukari. Namuuliza yakhe choo kitoke wapi huku? Namwangaliya komo langa'ra kwa kijassho chembamba.

Tukapiga kichochoro kimoja jamaa anvuta rasi hataki tena kwenda. Namuona pumzi matavuni
Anambiya, "Bwana hapa zitakharbatika!"
"Sasa itakuwaje" namuuliza
"Hakuna chakuwa hapa, nikukuojowa tu!"

Akalekeya ukuta na kufunguwa zipu. Hajajaza hata kikombe cha kahawa mara twasikiya

"Ai...oooh, ni nyinyi munatabiya kama ya umbwa?" Ndio hawa waitwao Kanjoo ama vipi?
"Ebu onyesha sisi choo na hapana rudisha exhibit ndani ya suruali!" Weeeeeh!.

Mimi niko? kubwaa. Namwacha jamaa yuko nyuma yuwaniandama mbio mikojo yamrukiya rukia aliya nimngojee.