Search This Blog

Friday, February 4, 2011

PILAU MOTO MOTO

Raha ya Ijumaa ni baada ya swalaa waenda piga pilau yako kwa kachumbari, pili pili ya kukaanga na jagi la juice. Hatupendi matanga lakini pia napo kuna pilau tamu!

Siku hiyo tulikwenda kuzika, baada ya mazishi tukarudi kulikofiliwa kupiga pilau yetu. Siniya zikaletwa moto moto. Ikawa siniya moja watu watatu. Nimekaa mimi, Mwamadi na Abduli

Pilau haidariki sura ilivyomoto lakini nikimwangaliya Abduli abugiya utasema ana friji mdomoni. Apiga matonge hakuna imani.



Mara twamuona Abduli amenyamaza kimya hali tena amwaga machozi tu. Wacha tuanze wasi wasi.

"Abduli una nini?" Jamaa wamuuliza.

Hajibu kitu azidi kuliya. Watu wakaanza wasi wasi kweli.

Baada ya kama dakika tano akafunguwa mdomo atwambiya kwa maskitiko "Poleni jamaa, kifo cha leo kimenikumbusha marhemu nyanyangu!"

Ikabidi tumsubirishe tumwambie ndio mambo ya kiduniya. Akanyamza akendeleya kula.

Tukitoka nje twaenda zetu mara anambiya "Wajua nini? Hakuna cha marhemu bibi wala ukwaju! Nilikuwa nimemenya kiazi moto kama kaa! Kimeniambata kwenye meno na mafinzi! Kukimiza siwezi na kukitema siwezi!"

No comments:

Post a Comment